Mbunge: Wabunge wanafiki
Mbunge wa Viti Maalum, Lucy Owenya amesema, wabunge wanaowashambulia mawaziri halafu wanaunga mkono hoja ni wanafiki.
Owenya amesema bungeni mjini Dodoma kuwa, wabunge hao wameapa katika mhimili huo wa dola hivyo wanapaswa kutimiza kiapo chao.
Mbunge huyo amesema, wabunge hao wamekuwa wakisema sana, wanawalalamikia sana mawaziri halafu wanaunga mkono hoja.
Wakati Owenya anazungumzia aliouita kuwa ni unafiki wa wabunge alisema wawakilishi hao wa wananchi hawawatendei haki mawaziri na alitumia vifungu vya Biblia kuhalalisha hoja yake.
Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene, alipinga kauli ya Mbunge huyo kwa madai kuwa kusema kuwa wabunge ni wanafiki ni kuwadhalilisha.
Simbachawene amesema bungeni kuwa, kauli ya Owenya inaudhi na inadhalilisha watu wengine hivyo akaomba mwongozo wa Mwenyekiti wa kikao cha Bunge, Zubeir Ali Maulid.
“Na sio kuunga mkono kwamba ni upungufu na unafiki” alisema Simbachawene wakati akimpinga Mbunge huyo aliyekuwa akichangia wakati wa mjadala wa bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2009/2010.
“Kalindwa na Biblia, asitumie tena lugha hiyo inaudhi”alisema Mwenyekiti wa Bunge.
Mvutano huo ulitokea muda mfupi kabla Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto kutakiwa kufuta usemi kwamba Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Jeremiah Sumari alijibu honyo hovyo hoja kuhusu kampuni ya Meremeta.
Hivi karibuni, Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii aliwashambulia mawaziri na kuwalaani kutokana na alichodai kuwa ni vitendo vyao vibaya.
Wabunge wamekuwa wakiwatuhumu mawaziri kuwa wanajipendelea na hawataki kuwahudumia wananchi wenye shida.
Wabunge hao wameahidi kumtajia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda majina ya mawaziri wasiotekeleza wajibu wao na wanaokiuka misingi ya utawala bora.
Wabunge hao wamemsifu Waziri Mkuu kuwa ni muadilifu, na ana hofu ya Mungu. Mjadala wa bajeti hiyo iliyowasilishwa bungeni Jumatatu utahitimishwa leo.
Kwa mujibu wa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kabla wabunge hawajaanza kuchangia bajeti hiyo, zaidi ya wabunge 100 waliomba kuchangia lakini kwa sababu ya muda, takribani wabunge sitini tu ndiyo wangepata nafasi hiyo.